UFAFANUZI KUHUSU KUPITIWA UPYA KWA MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012
Mnamo tarehe 03 Mei, 2013 Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Wiliam Lukuvi (Mb) ilitoa Kauli ya Serikali
Bungeni Kuhusu Taarifa ya Awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Sababu za
kushuka kwa ufaulu wa Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012.
Kauli ya Serikali ilielekeza kuwa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato
cha Nne mwaka 2012 yafutwe na yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu
uliotumika mwaka 2011 ili Wanafunzi hao wawe katika mazingira
yanayofanana na ya wenzao wa miaka iliyopita kwa kuwa mfumo uliotumika
mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule
uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia.
Kwa kuzingatia
mapendekezo ya Tume na Maelekezo ya Baraza la Mawaziri, Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, kwar mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Baraza
la Mitihani Tanzania, kifungu cha 20, sura 107 ameliagiza Baraza la
Mitihani la Taifa kupitia upya Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne
mwaka 2012.
Aidha, imeagizwa kwamba matokeo hayo yaandaliwe kwa
kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011. Serikali haikuagiza kufanyika
upya kwa mitihani hiyo na wala haikuagiza kusahihishwa upya. Hivyo,
Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba hapatakuwa na zoezi la
kurudia usahihishaji wa mtihani huo kwa sababu hakuna dosari
zilizobainishwa kwenye usahihishaji wa mitihani hiyo.
Alama za
watahiniwa ambazo zimehakikiwa zipo tayari, kitakachofanyika ni kwa
Baraza la Mitihani kutumia alama hizo kuchakata matokeo upya kwa kutumia
viwango vya ufaulu vilivyotumika mwaka 2011. Utaratibu ambao umekuwa
ukitumika tangu mwaka 1973 wakati Baraza lilipoanzishwa, ni wa kuweka
viwango vya ufaulu kila mwaka kwa kuzingatia ufaulu wa somo husika na
ufaulu katika mwaka uliotangulia.
Kutokana na maelezo hayo, ni
dhahiri kuwa zoezi la kupitia upya matokeo ya Kidato cha Nne 2012
litachukua muda mfupi na matokeo yatatangazwa hivi karibuni.
Selestine Gesimba
KAIMU KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI 10/05/2013
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment