Skip to main content

MASAA 24 YA MLEMAVU WA MACHO UDSM!







Pichani ni Vicent Mzena(Mwenye fimbo nyeupe)
 MASAA 24 YA MLEMAVU WA MACHO UDSM!
Hi sehemu ya makala yangu kwenye gazeti la RAI no 978

...... Binafsi sipingi kuanzishwa kwa mfumo shirikishi. Kwa mtazamo wangu, mfumo shirikishi una faida anuai. Mosi, unawaandaa wanafunzi walemavu kuchanganyika na jamii ambayo kimsingi ndiyo wataishi nayo uraiani. Pili, unawapa fursa wanafunzi wasio walemavu kufahamu changamoto, fursa na mahitaji ya walemavu. Pia mfumo shirikishi unasemwa kuongeza fursa kwa walemavu wengi zaidi kupata elimu kwa sababu una gharama nafuu. Hili la mwisho linahitaji utafiti zaidi.
Jambo la msingi ambalo tunapaswa kujiuliza ni kama wanafunzi wasio na ulemavu na jamuiya za taasisi za elimu kama vile shule na vyuo zimejiandaa kikamilifu kuishi kwa upendo na walemavu na kufahamu vyema mahitaji yao. Nasema hivyo kwa sababu elimu shirikishi haiwezi kufanikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa kama jamii itakuwa haijaandaliwa vizuri kisaikolojia kuwapokea, kuwajali na kuwapenda walemavu.
Leo tutazame jinsi mfumo shirikishi unavyofanya kazi kwa mfano halisi; mfano wa maisha yangu. Mwaka 2011 ulikuwa mwaka wa mafanikio makubwa kwangu kwenye siasa za chuo kikuu. Kwanza nilichaguliwa kuwa Katibu wa kitivo cha sheria na baadaye katibu wa bodi ya serikali ya wanafunzi(DARUSO). Kiongozi wa nafasi hiyo, ana fursa kubwa ya kupata sehemu nzuri ya malazi kwenye hosteli za chuo.
Mimi niliamua kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho Vicent Mzena ambaye naye alikuwa waziri wa Jinsia na makundi maalum katika serikali ya wanafunzi(DARUSO). Kuipokea changamoto ya kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho kumenipa ‘’uamsho’’ mkubwa. Mzena amekuwa mwalimu wangu mkubwa kuhusu mambo ya walemavu.
Somo la kwanza: Hapa tunajifunza kwamba jamii inapaswa kuchukulia kwamba kuishi na walemavu sio tatizo bali ni changamoto inayozalisha fursa ya kujifunza zaidi kutoka kwa walemavu na kuonyesha upendo kwao.
Ni asububuhi kumeshapambazuka. Mzena anaamka mapema. Chumba kimepangiliwa vyema na anafahamu ulipo mswaki, dawa ya meno na maji. Anakwenda mwenyewe bafuni kusafisha mwili. Mimi naamka na kumsaidia kunyoosha nguo zake alizozifua jana. Mzena ana desturi ya kufua nguo mwenyewe na kufuliwa mara chache hasa anapotingwa na majukumu.
Somo la pili: Hapa tunajifunza kwamba katika mfumo shirikishi, kila mmoja ana jukumu la kutekeleza. Walemavu wanapaswa kujizoesha kufanya wenyewe kazi ndogondogo wanazozimudu. Pia wanajamii wanaowazunguka walemavu wanajukumu la kuwasaidia kufanya kazi wasizoweza kuzitekeleza wenyewe.
Namshika mkono Mzena kumpeleka darasani ambaye mkononi ana fimbo nyeupe na begi la vifaa vya shule. Madarasa yako mbali kiasi. Mzena ni mcheshi sana. Tunacheka njia nzima huku akinitania kuwa mimi ni ‘’dereva mahiri’’. UDSM kuna jiografia ya milima lakini Mzena anajitahidi kuyazoea mazingira japo hapa na pale anatatizwa na ngazi.
Somo la nne: Hapa tunajifunza kwamba shule za mchanganyiko wa walemavu na watu wengine ziwe na miundombinu na mazingira rafiki kwa walemavu. Lakini pia walemavu wana jukumu la kuikabili changamoto ya mazingira yao kadiri inavyowezekana.

Kwenye varanda za hosteli na njiani kuelekea darasani tunakutana na wanafunzi wenzetu. Wanaonyesha kutujali na kutupisha njiani upesi. Lakini hapa kuna jambo la kuongeza. Wengi wanaonyesha kutunduwaa kwa mshangao. Baadhi yao wanasimamisha mazungumzo yao. Kwa ufupi,licha ya kuonyesha upendo na kujali, kuna kila dalili kwamba bado hawajaizoea kiukamilifu hali ya kujichanganya na walemavu.
Somo la tano: Hapa tunajifunza umuhimu wa kuijenga jamii kisaikolojia ili iweze kuwapokea walemavu kama sehemu ya jamii.
Sasa ni wakati wa kula. Mimi na mzena tunajongea kafeteria kupata staftahi. Kuna msururu mrefu wa wanafunzi. Awali, walemavu walipaswa kupanga foleni kama watu wengine. Baada ya jitihada za viongozi wa walemavu, sasa walemavu wanahudumiwa vizuri na wahudumu wa cafeteria.
Somo la sita: kwenye foleni na misururu inayochosha kama vile benki, mIgahawani, kwenye vyombo vya usafiri na hospitali, walemavu wapewe kipaumbele.
Ni usiku na giza linachukua sehemu yake. Mimi, Mzena na marafiki wengine tuko chumbani tukibadilishana mawazo. Ghafla anaingia Maingu Nyanjila, mwanamke aliyejitolea vya kutosha kwa ajili ya walemavu. Amekuja kumchukua Mzena akamsomee kitabu cha fasihi, ‘’Autobiography of Malcom X’’. Ni kitabu kikubwa lakini Mzena hana namna isipokuwa kumsikiliza Maingu akimsomea kurasa moja hadi nyingine. Hakuna vitabu katika maandishi maalumu ya nukta nundu(Braille). Vingekuwepo Mzena asingehitaji mtu wa kumsomea. Baadhi ya walimu wa chuo wanawapa walemavu notisi zao ambazo mzena anazisoma kwa vifaa vya kielektroniki vya kutunzia kumbukumbu au kompyuta yenye programu ya sauti. Darasani anapaswa kwenda na tepurekoda inayonasa mafundisho ya mwalimu. Kwa bahati mbaya, si kila kitu kinasemwa kwa sauti; baadhi ya mambo yanaandikwa ubaoni bila kuzungumzwa.

Somo la saba: Katika dunia ya leo ya kielektroniki, kuna vifaa vingi ambavyo vinaifanya elimu ya walemavu iwe rahisi na yenye tija. Jamii na wadau wote wa haki za walemavu wajitahidi kufadhili upatikanaji wa vifaa muhimu.
Kabla hawajaondoka chumbani kwenda maktaba au darasani kujisomea, ni desturi ya Maingu kuibua mjadala kuhusu mada ya kijamii. Ni vijana kutoka fani mbalimbali na kila mmoja analeta hoja yake. Mzena anatoa hoja kwa mtazamo wa kielimu na mimi naleta vifungu vya sheria. Maingu anaingilia na kutoa hoja ya kifasihi. Mara nyingi wanajua jinsi ya kunishinda. ’’Nyinyi wanasheria muna maneno mengi na hamtakwenda mbinguni kwa sababu hamtendi haki’’ Maingu angenitania ili kuidhoofisha hoja yangu.
Somo la nane: Walemavu washiriki kwenye mijadala ya kila siku ya makundirika. Marafiki wawape walemavu nafasi ya kutoa hoja zao na kuheshimu mitizamo yao. Walemavu wana tafakuri kama walivyo watu wengine.
Kuna mengi ya kuyazungumza kuhusu elimu shirikishi. Shule ya Msingi Nanjoka na Sekondari ya Frankweston nilikuwa swahibu wa mwanafunzi mwenzangu ambaye alikuwa mlemavu wakusikia. Ndanda nilisoma na walemavu wa macho. UDSM nimekutana na walemavu wa kila namna. Lakini, darasa maridhawa nimelipata nilipokata shauri kuishi na vicent Mzena, mlemavu wa macho. Natamani walemavu wote wangekuwa na moyo kama wa Mzena. Pia, nawausia vijana wenzangu na wanajamii kwa ujumla kuishi, kujenga urafiki na kuwakaribisha walemavu.
Lakini hali ikoje kwenye jamii? Utafiti uliofanywa na kituo cha taarifa kuhusu ulemavu( Information Centre on Disability-ICD) katika Manispaa ya Moshi, Mwanza na Morogoro kuhusu mchangamano baina ya walemavu na watu wasio na ulemavu, unaonyesha kuwa bado kuna changamoto katika kufanikisha mfumo shirikishi. Utafiti huo unaonyesha kwamba asilimia 57 ya watu kutokuwa na utayari na kukosa hulka ya upendo kwa walemavu wakati ni asilimia 47 tu ya watu ilionyesha kuwa na moyo wa kuwajali, kuwapenda na kuwakaribisha walemavu. Shime wanajamii tuibadili hali hii na kuishi kwa upendo na walemavu.
Inawezekana.Fanya tafakuri ya kina kisha chukua hatua.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba ya simu 0653619906. Barua pepe adoado75@hotmail.com

SOURCE :  http://www.facebook.com/ado.shaibu.3/posts/545137165537310

Comments

Popular posts from this blog

SOMO LA TATU : UTENGENEZAJI WA UNGA LISHE.

Mahindi   ni  miongoni  mwa  mazao ya  chakula  ambayo  unga  wake  unatumika  kutengeneza    unga  lishe. UNGA  LISHE  :  Ni  unga  bora  na  unao  hitajika  sana  katika  kuborehs  afya  za  watoto, wazee  na  wagonjwa.  Ukiwa  kama  mjasiriamali  mdogo, ni  muhimu  kujua  namna  ya  kutengeneza  unga  lishe, kwani  malighafi  zinazo  tumika  katika  utayarishaji  wa  unga  huu  zinapatikana  kwa  wingi  na  kwa  bei  nafuu, hivyo  basi  hata  kwa  wewe  mwenye  mtaji  mdogo,  unaweza   kufanya  biashara  hii   bila  ya  kuhitajika  kuwa  na  mtaji  mkubwa  jambo  linalo  chukuliwa  kama  changamoto  kwa  wajasiriamali wengi  nchini. MCHELE. MALIGHAFI  ZINAZO  HITAJIKA  KATIKA  UTENGENEZAJI  WA  UNGA  LISHE. * Karanga    - Nusu  Kilo. * Soya         - Nusu  Kilo. * Ulezi         -   Kilo  moja  na  Nusu. * Mahindi    -Nusu  Kilo *Mtama     - Mtama  Nusu  Kilo. * Uwele     -  Nusu  kilo. * Mchele    -  Nusu  kilo.. JINSI  YA  KUTENGENEZA  UNGA  LISHE . 1. S

NAFASI ZA KUJITOLEA SINGIDA

Taasisi  ya  ORPHANS  &  VULNARABLE   CHILDREN  CARE    (  OVCC  )  ya  Mjini  SINDIDA  inatangaza  nafasi  za  kazi  za  kujitolea  kama  ifuatavyo  : Picha  za  matukio  ya  shughuli  mbalimbali  za  Taasisi  ya OVCC.   1.       Miandi Secondary school:-       Volunteers wa masomo yafuatayo:-          (i) Physics               2          (ii) Chemistry           2          (iii) Biology              2          (iv) Geography         1          (v) Basic Mathematics. 2 2.         Puma Secondary School:-       Volunteers wa masomo yafuatayo:-         (i) Fnglish                        2         (ii) Physics                      3         (iii) Chemistry                  3                        (iv) Biology                      3         (v) Basic Mathematics     4 3.       Puma Dispensary:-     Volunteers wa Taaluma zifuatazo:-       (i) Taaluma ya Utabibu             8       (ii) Taaluma ya Kinga ya Afya   8

SOMO LA NANE : KUTENGENEZA WINE YA NANASI.

Nanasi.  Wine  ya  nanasi  ni  rahisi  kutengeneza  kwa  sababu  mananasi  yanapatikana  kwa  wingi  sana  katika  kipindi  kirefu  cha  mwaka. MALIGHAFI  ZINAZO  HITAJIKA  KATIKA  UTENGENEZAJI  WA  WINE  YA  NANASI. * Nanasi. *  Maji. * Sukari. * Amira. HATUA  YA  KWANZA  KUTENGENEZA *  Menye  maganda  ya  mananase  na  kupata  nyama . ( Kinacho  tumika  katika  utengenezaji  wa  wine  ya  nanasi  ni  nanasi  lenyewe  na  sio  maganda  ya  mananasi  ) *  Katakata  vipande  vidogo  kisha  weka  katika  chombo  kwa  ajili  ya  kuchemsha,  nanasi  linalo  faa  katika  utengenezaji  wa  wine  ya  nanasi  ni  nanasi  lenye  uzito  wa  kg. 5. * Chemsha  kwa  muda  wa  dakika  30  kwa  moto  wa  kawaida (  Inashauriwa  kutumia  moto  wa  mkaa  ) * Baada  ya  kupoa   anza kuchachua  kwa  kuweka  amira   vijiko  vinne (  4  )  vya  chakula ,  sukari  vijiko  viwili  vya  chai na  kisha  koroga  kwa  muda  wa  dakika  20. *  Acha  kwa  muda  wa  dakika  5  ukiwa  una