Total Pageviews

Monday, December 29, 2014

Kutana na kinyozi anayemiliki magari 75

New Delhi. Mfanyabiashara Leonard Willoughby aliwahi kusema; ‘siku utakayoanza kuishi kwa kuifuata mipango yako unayopanga, kila kitu katika maisha yako kitabadilika kabisa.’ Inawezekana watu wengi wanaufahamu msemo huo, lakini Ramesh Babu anajitapa kuyatendea kazi maneno hayo.
Babu ambaye ni kinyozi bilionea pekee nchini India, anasema aliuchukua ushauri wa Willoughby na kuamua kuutendea kazi tangu siku ya kwanza alipousikia na kwamba maisha yake yalianza kubadilika.
Kwa mujibu wa Jarida la ‘Your story’ la nchini India, Babu amefanikiwa kuvuka vizingiti kadhaa vya umaskini hadi kufikia kuwa mmoja wa watu maarufu nchini humo akiwa na uwezo wa kununua gari aina yoyote anayoitaka.
Asema kuwa mwaka 1994 alinunua gari lake la kwanza aina ya Maruti, lakini aliendelea na kuhifadhi fedha kidogo kidogo alizokuwa anazipata hadi mwaka 2004, alipoanzisha kampuni ya kokodisha magari, ikiwa na magari saba wakati huo.
Hadi kufikia mwaka huu, kinyozi huyo amelinunua magari 75 kati ya hayo matano ni ya kifahari yakiwemo, Mercedes, BMW, Audi, mabasi kumi na lile analolipenda liitwalo Rollsw Royce.
Pamoja na utajiri huo mkubwa alionao Babu, bado anaendelea na kazi yake ya kinyozi. Akisimulia maisha yake ya awali, anasema kuwa alizaliwa katika familia masikini, baba yake alikuwa kinyozi na kwamba alifariki mwaka 1979 wakati Babu akiwa na miaka saba.
“Baba yangu alituachia biashara ya saluni Mtaa wa Brigade ambalo mjomba wangu alichukua akaanza kuiongoza. Anawa anatupa kiasi kidogo cha fedha. Tulikuwa tunakula chakula kimoja kwa siku ili tuweze kuishi tu,” anasimulia.
Anasema alipokuwa shule ya msingi, alilazimika kufanya kazi ili kuweza kujikimu kimaisha kwa kupata kiasi kidogo cha fedha.
“Nilikuwa nikibeba magazeti na chupa za maziwa na kitu kingine chochote ambacho kingeweza kupunguza ugumu wa maisha ya mama yangu. Hii ndiyo sababu ya kuhitimu masomo yangu,” anasema.
Baadaye alifanikiwa uendelea na masomo yake, jambo lililomfanya mama yake aanzishe ugomvi na mjomba aliyekuwa akisimamia duka baada ya kugoma kutoa fedha za matumizi.
“Ndipo nilipomwambia mama nitachukua saluni na kukiendesha mwenyewe. Hakupenda uamuzi huo kwa kuwa alifikiri nitaacha masomo, lakini nilianza kazi hiyo.
“Asubuhi nilikuwa saluni, jioni nilikwenda masomoni kisha usiku nilikuwa saluni tena na kufanya kazi hadi saa 7 usiku. Hivyo ndivyo nilivyoanza kuitwa kinyozi,” anasema.
Milango ya baraka inafunguka
Mwishoni mwa mwaka 1993, Babu alinunua gari la mtumba aina ya Maruti Van. Kwa kuwa mjomba wangu alikuwa ameshanunua gari moja alinishawishi na mimi kununua.ilibidi babu yangu aweke nyumba yake dhamana nini nimchukue mkopo.
“Binti katika nyumba ambayo mama yangu alikuwa akifanya kazi, aliniuliza kwa nini sikodishi gari badala yake naliegesha tu nyumbani. Alinifundisha namna ya kusimamia biashara hiyo, kwangu alikuwa kama dada yangu,” anasimulia.
Kuanzia mwaka 1994 ndipo Babu alipojiingiza rasmi kwenye biashara ya kukodisha magari. Magari ya kwanza niliyapata katika Kampuni ya Intel, alikokuwa anafanya kazi Nandini Akka.
“Taratibu nilianza kuongeza magari kwenye yadi yangu. Kufikia mwaka 2004 nilikuwa na magari sita tu, biashara ilikuwa haifanyi vizuri kutokana na ushindani mkali uliokuwapo.
“Kwa sababu kila mtu alikuwa na magari madogo ya kawaida, nilitaka ninunue magari ya kifahari kupunguza ushindani,” anasema.
Babu anasema siku aliponunua gari lake la kwanza la kifahari mwaka 2004, kila mtu alimwambia kuwa amefanya kosa kubwa. Niliogopa lakini sikuwa na namna zaidi ya kuendelea na mpango wangu.
“Nilijiambiwa mwenyewe kuwa ningeuza magari kama hali ingekuwa mbaya. Bahati nzuri kwangu biashara ililipa sana. Nilikuwa mtu wa kwanza katika Bangalore yote kuagiza magari ya kifahari mapya,” anasema.
Babu anasema kama unataka kufanya biashara lazima uwe tayari kukabiliana ana hatari yoyote itakayojitokeza, wakati akinunua Rolls Royce mwaka 2011 rafiki zake walimwonya kuwa anacheza ‘kamali’ na biashara yake.
“Niliwaambia nilishajitosa mwaka 2004, kwa nini nisijaribu tena miaka kumi baadaye? Ilinigharibu fedha nyingi, lakini kama ilivyokuwa mwanzo biashara ililipa sana” anasema.
Changamoto
Changamoto kubwa kwake ni gharama za kulipa kodi ya ushuru wa barabara, kiasi kwamba sijui jambo hilo nilifanyaje.
Babu asema mwanzoni wakati anaanza kufanya biashara ya magari alikuwa akilipa kodi kila baada ya miezi minne, lakini sasa atalazimika kubadili utaratibu huo kwa kuwa kodi zimekuwa kubwa mno kiasi kwamba zinaweza ‘kumvurugia’ mpango wake wa kununua magari ya Limousines na mengine ya kifahari mwaka 2015.
Babu anawaambia watu wanaotaka kuwa kama yeye: “Fanya kazi kwa bidii, kuwa mcheshi, mambo mengine yanayobaki ni bahati tu.”
Kuhusu ndoa yake
Babu ameoa na ana watoto watatu, wote wakiwa ni wanafunzi. Watoto wawili wa kwanza ni wasichana, mtoto wa mwisho ni mvulana.
“Nitawafundisha watoto wangu kufanya kazi zangu zote mbili (kunyoa na kukodisha magari),” anasema Babu.
Babu anasifika kwa kutokuwa mwanachama wa klabu yoyote kwa kile anachosema kuwa hana nafasi ya kujihusisha na mambo hayo.
Kinyozi huyo hupenda kuitumia Jumapili yote katika saluni yake, jambo linalomaanisha kuwa hana kitu anachokiita ‘mapumziko’.
Amewahi kusafiri kwenda Ujerumani kama mtalii na Singapore kwa ajili ya kwenda kujifunza kunyoa nywele za wanawake.
Imeandaliwa na Goodluck Eliona kwa msaada wa mtandao

CREDIT :  GAZETI  LA  MWANANCHI, DESEMBA  28, 2014.

No comments:

Post a Comment