Total Pageviews

Thursday, April 11, 2013

MASAA 24 YA MLEMAVU WA MACHO UDSM!Pichani ni Vicent Mzena(Mwenye fimbo nyeupe)
 MASAA 24 YA MLEMAVU WA MACHO UDSM!
Hi sehemu ya makala yangu kwenye gazeti la RAI no 978

...... Binafsi sipingi kuanzishwa kwa mfumo shirikishi. Kwa mtazamo wangu, mfumo shirikishi una faida anuai. Mosi, unawaandaa wanafunzi walemavu kuchanganyika na jamii ambayo kimsingi ndiyo wataishi nayo uraiani. Pili, unawapa fursa wanafunzi wasio walemavu kufahamu changamoto, fursa na mahitaji ya walemavu. Pia mfumo shirikishi unasemwa kuongeza fursa kwa walemavu wengi zaidi kupata elimu kwa sababu una gharama nafuu. Hili la mwisho linahitaji utafiti zaidi.
Jambo la msingi ambalo tunapaswa kujiuliza ni kama wanafunzi wasio na ulemavu na jamuiya za taasisi za elimu kama vile shule na vyuo zimejiandaa kikamilifu kuishi kwa upendo na walemavu na kufahamu vyema mahitaji yao. Nasema hivyo kwa sababu elimu shirikishi haiwezi kufanikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa kama jamii itakuwa haijaandaliwa vizuri kisaikolojia kuwapokea, kuwajali na kuwapenda walemavu.
Leo tutazame jinsi mfumo shirikishi unavyofanya kazi kwa mfano halisi; mfano wa maisha yangu. Mwaka 2011 ulikuwa mwaka wa mafanikio makubwa kwangu kwenye siasa za chuo kikuu. Kwanza nilichaguliwa kuwa Katibu wa kitivo cha sheria na baadaye katibu wa bodi ya serikali ya wanafunzi(DARUSO). Kiongozi wa nafasi hiyo, ana fursa kubwa ya kupata sehemu nzuri ya malazi kwenye hosteli za chuo.
Mimi niliamua kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho Vicent Mzena ambaye naye alikuwa waziri wa Jinsia na makundi maalum katika serikali ya wanafunzi(DARUSO). Kuipokea changamoto ya kuishi chumba kimoja na mlemavu wa macho kumenipa ‘’uamsho’’ mkubwa. Mzena amekuwa mwalimu wangu mkubwa kuhusu mambo ya walemavu.
Somo la kwanza: Hapa tunajifunza kwamba jamii inapaswa kuchukulia kwamba kuishi na walemavu sio tatizo bali ni changamoto inayozalisha fursa ya kujifunza zaidi kutoka kwa walemavu na kuonyesha upendo kwao.
Ni asububuhi kumeshapambazuka. Mzena anaamka mapema. Chumba kimepangiliwa vyema na anafahamu ulipo mswaki, dawa ya meno na maji. Anakwenda mwenyewe bafuni kusafisha mwili. Mimi naamka na kumsaidia kunyoosha nguo zake alizozifua jana. Mzena ana desturi ya kufua nguo mwenyewe na kufuliwa mara chache hasa anapotingwa na majukumu.
Somo la pili: Hapa tunajifunza kwamba katika mfumo shirikishi, kila mmoja ana jukumu la kutekeleza. Walemavu wanapaswa kujizoesha kufanya wenyewe kazi ndogondogo wanazozimudu. Pia wanajamii wanaowazunguka walemavu wanajukumu la kuwasaidia kufanya kazi wasizoweza kuzitekeleza wenyewe.
Namshika mkono Mzena kumpeleka darasani ambaye mkononi ana fimbo nyeupe na begi la vifaa vya shule. Madarasa yako mbali kiasi. Mzena ni mcheshi sana. Tunacheka njia nzima huku akinitania kuwa mimi ni ‘’dereva mahiri’’. UDSM kuna jiografia ya milima lakini Mzena anajitahidi kuyazoea mazingira japo hapa na pale anatatizwa na ngazi.
Somo la nne: Hapa tunajifunza kwamba shule za mchanganyiko wa walemavu na watu wengine ziwe na miundombinu na mazingira rafiki kwa walemavu. Lakini pia walemavu wana jukumu la kuikabili changamoto ya mazingira yao kadiri inavyowezekana.

Kwenye varanda za hosteli na njiani kuelekea darasani tunakutana na wanafunzi wenzetu. Wanaonyesha kutujali na kutupisha njiani upesi. Lakini hapa kuna jambo la kuongeza. Wengi wanaonyesha kutunduwaa kwa mshangao. Baadhi yao wanasimamisha mazungumzo yao. Kwa ufupi,licha ya kuonyesha upendo na kujali, kuna kila dalili kwamba bado hawajaizoea kiukamilifu hali ya kujichanganya na walemavu.
Somo la tano: Hapa tunajifunza umuhimu wa kuijenga jamii kisaikolojia ili iweze kuwapokea walemavu kama sehemu ya jamii.
Sasa ni wakati wa kula. Mimi na mzena tunajongea kafeteria kupata staftahi. Kuna msururu mrefu wa wanafunzi. Awali, walemavu walipaswa kupanga foleni kama watu wengine. Baada ya jitihada za viongozi wa walemavu, sasa walemavu wanahudumiwa vizuri na wahudumu wa cafeteria.
Somo la sita: kwenye foleni na misururu inayochosha kama vile benki, mIgahawani, kwenye vyombo vya usafiri na hospitali, walemavu wapewe kipaumbele.
Ni usiku na giza linachukua sehemu yake. Mimi, Mzena na marafiki wengine tuko chumbani tukibadilishana mawazo. Ghafla anaingia Maingu Nyanjila, mwanamke aliyejitolea vya kutosha kwa ajili ya walemavu. Amekuja kumchukua Mzena akamsomee kitabu cha fasihi, ‘’Autobiography of Malcom X’’. Ni kitabu kikubwa lakini Mzena hana namna isipokuwa kumsikiliza Maingu akimsomea kurasa moja hadi nyingine. Hakuna vitabu katika maandishi maalumu ya nukta nundu(Braille). Vingekuwepo Mzena asingehitaji mtu wa kumsomea. Baadhi ya walimu wa chuo wanawapa walemavu notisi zao ambazo mzena anazisoma kwa vifaa vya kielektroniki vya kutunzia kumbukumbu au kompyuta yenye programu ya sauti. Darasani anapaswa kwenda na tepurekoda inayonasa mafundisho ya mwalimu. Kwa bahati mbaya, si kila kitu kinasemwa kwa sauti; baadhi ya mambo yanaandikwa ubaoni bila kuzungumzwa.

Somo la saba: Katika dunia ya leo ya kielektroniki, kuna vifaa vingi ambavyo vinaifanya elimu ya walemavu iwe rahisi na yenye tija. Jamii na wadau wote wa haki za walemavu wajitahidi kufadhili upatikanaji wa vifaa muhimu.
Kabla hawajaondoka chumbani kwenda maktaba au darasani kujisomea, ni desturi ya Maingu kuibua mjadala kuhusu mada ya kijamii. Ni vijana kutoka fani mbalimbali na kila mmoja analeta hoja yake. Mzena anatoa hoja kwa mtazamo wa kielimu na mimi naleta vifungu vya sheria. Maingu anaingilia na kutoa hoja ya kifasihi. Mara nyingi wanajua jinsi ya kunishinda. ’’Nyinyi wanasheria muna maneno mengi na hamtakwenda mbinguni kwa sababu hamtendi haki’’ Maingu angenitania ili kuidhoofisha hoja yangu.
Somo la nane: Walemavu washiriki kwenye mijadala ya kila siku ya makundirika. Marafiki wawape walemavu nafasi ya kutoa hoja zao na kuheshimu mitizamo yao. Walemavu wana tafakuri kama walivyo watu wengine.
Kuna mengi ya kuyazungumza kuhusu elimu shirikishi. Shule ya Msingi Nanjoka na Sekondari ya Frankweston nilikuwa swahibu wa mwanafunzi mwenzangu ambaye alikuwa mlemavu wakusikia. Ndanda nilisoma na walemavu wa macho. UDSM nimekutana na walemavu wa kila namna. Lakini, darasa maridhawa nimelipata nilipokata shauri kuishi na vicent Mzena, mlemavu wa macho. Natamani walemavu wote wangekuwa na moyo kama wa Mzena. Pia, nawausia vijana wenzangu na wanajamii kwa ujumla kuishi, kujenga urafiki na kuwakaribisha walemavu.
Lakini hali ikoje kwenye jamii? Utafiti uliofanywa na kituo cha taarifa kuhusu ulemavu( Information Centre on Disability-ICD) katika Manispaa ya Moshi, Mwanza na Morogoro kuhusu mchangamano baina ya walemavu na watu wasio na ulemavu, unaonyesha kuwa bado kuna changamoto katika kufanikisha mfumo shirikishi. Utafiti huo unaonyesha kwamba asilimia 57 ya watu kutokuwa na utayari na kukosa hulka ya upendo kwa walemavu wakati ni asilimia 47 tu ya watu ilionyesha kuwa na moyo wa kuwajali, kuwapenda na kuwakaribisha walemavu. Shime wanajamii tuibadili hali hii na kuishi kwa upendo na walemavu.
Inawezekana.Fanya tafakuri ya kina kisha chukua hatua.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba ya simu 0653619906. Barua pepe adoado75@hotmail.com

SOURCE :  http://www.facebook.com/ado.shaibu.3/posts/545137165537310

No comments:

Post a Comment